Tech news

Google Yalipa Fidia ya Kihistoria kwa Matumizi Mabaya ya Data

Google Yalipa Fidia ya Kihistoria kwa Matumizi Mabaya ya Data

Kampuni ya teknolojia ya Google imekubali kulipa fidia ya jumla ya dola milioni 314.6 (sawa na takriban shilingi bilioni 40 za Kenya) kwa watumiaji wa Android katika jimbo la California, Marekani, kufuatia madai ya matumizi mabaya ya data za binafsi.

Makubaliano hayo ni sehemu ya suluhu ya kesi ya pamoja iliyowasilishwa mahakamani dhidi ya kampuni hiyo, ambapo ilidaiwa kuwa Google ilikusanya na kutumia taarifa za mahali walipo watumiaji bila ridhaa yao halali.

Kwa mujibu wa hati za mahakama zilizotolewa wiki hii, Google ilituhumiwa kwa kushindwa kutoa taarifa za kutosha kwa watumiaji kuhusu jinsi taarifa zao za mahali zinavyokusanywa na kutumiwa kupitia huduma zake mbalimbali, ikiwemo Google Maps na Google Search, hata baada ya watumiaji kuzima huduma za ufuatiliaji wa eneo (location tracking).

Mwendesha mashtaka mkuu wa jimbo la California, Rob Bonta, alisema kwamba makubaliano hayo ni ushindi mkubwa kwa haki za faragha za watumiaji.

Kwa mujibu wa mkataba wa fidia hiyo, zaidi ya wakazi milioni nne wa California wanaostahili walengwa wa fidia hiyo na wataarifiwa jinsi ya kudai malipo yao. Hata hivyo, kiwango halisi ambacho kila mtumiaji atapokea kitapangwa kulingana na idadi ya waliotimiza masharti ya madai.

Hii si mara ya kwanza kwa Google kulazimika kulipa fidia kutokana na masuala ya faragha. Mwaka 2022, kampuni hiyo ililipa dola milioni 391 kwa majimbo 40 ya Marekani kutokana na tuhuma kama hizo.

Google bado haijatoa taarifa rasmi kuhusu makubaliano haya mapya, lakini imekuwa ikijitetea kwamba imeboresha sera zake za faragha na kuwapa watumiaji wake udhibiti zaidi wa taarifa zao binafsi.