Sports news

Harambee Stars Yaondolewa CHAN Baada ya Kipigo Kutoka Madagascar

Harambee Stars Yaondolewa CHAN Baada ya Kipigo Kutoka Madagascar

Timu ya taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars, imetamatisha safari yake katika mashindano ya CHAN 2024 baada ya kupoteza kwa mikwaju ya penalti 4-3 dhidi ya Madagascar, katika robo fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Moi Kasarani, Nairobi.

Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya 1-1 katika muda wa kawaida na muda wa nyongeza. Alphonce Omija aliwapa Wakenya matumaini kwa kufunga bao la kuongoza dakika ya 48, kabla ya Madagascar kusawazisha dakika ya 70 kupitia penalti ya Fenohazina Razafimaro. Kenya ilionekana kufunga bao la pili kupitia Ryan Ogam, lakini bao hilo lilikataliwa na mwamuzi Adelbert Diouf kutoka Senegal, kwa madai ya faulo iliyotangulia.

Katika mikwaju ya penalti, Madagascar ilifunga kupitia kwa Randriamanampisoa, Rafanomezantsoa, Razafimaro, na Rakotondraibe, huku Randrianirina akikosa. Kwa upande wa Kenya, Mohammed Siraj, Daniel Sakari, na Sylvester Owino walifunga penalti zao, lakini Alphonce Omija na Mike Kibwage walikosa.

Mashindano ya robo fainali yanaendelea leo ambapo Uganda, ambao ni wenyeji mwenza, watakutana na mabingwa watetezi Senegal, huku Sudan ikimenyana na Algeria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *