
Sosholaiti na mfanyabiashara maarufu wa Kenya, Huddah Monroe, ameibua mjadala mitandaoni baada ya kupandisha bei ya ofa yake ya lunch date kutoka KSh 50,000 hadi KSh 150,000. Hatua hiyo inadaiwa kuchochewa na uhitaji mkubwa kutoka kwa mashabiki wanaotaka kukutana naye.
Kupitia tangazo lake, Huddah alisema mpango huo unalenga kutoa nafasi kwa mashabiki wake waliotamani muda mrefu kupata muda wa ana kwa ana naye. Aidha, alidai kuwa malipo hayo yamekuwa mengi kiasi cha kufanya akaunti yake ya M-Pesa kufurika.
Awali, Huddah alikuwa ameeleza kuwa gharama ya lunch date ilikuwa KSh 50,000, lakini sasa imeongezwa mara tatu. Vilevile, aliongeza kuwa kwa mtu anayetaka kuwa rafiki wake wa karibu, atatakiwa kulipia kiasi cha KSh 1 milioni.
Tangazo hilo limeendelea kuvutia hisia mseto, mashabiki wengine wakimpongeza kwa kuthamini muda wake, huku wengine wakipinga bei hizo wakiziona kama kupita kiasi.