Mtandao wa kijamii wa Instagram umeanza kufanya mabadiliko mapya katika mwonekano wa Navigation Bar ile sehemu ya chini ya programu ili kurahisisha matumizi na kuboresha uzoefu wa watumiaji.
Katika mwonekano mpya, Instagram imepanga upya baadhi ya vipengele muhimu kama ifuatavyo:
Sehemu ya DM (Direct Messages) itahamishwa chini, jambo litakaloiwezesha kuonekana kwa urahisi zaidi na kufikiwa haraka na watumiaji. Sehemu ya kuweka post mpya (+) sasa itakuwa juu kushoto badala ya kuwa katika Navigation Bar ya chini. Hii inamaanisha alama ya “+” haitakuwepo tena kwenye sehemu ya chini ya skrini.
Logo ya Instagram itahamishwa kutoka upande wa kushoto na sasa itaonekana katikati ya skrini, ikitoa mwonekano wa kisasa zaidi. Watumiaji watakapofungua Home, badala ya kuona picha pekee, sasa wataanza kuona video za Reels, sawa na mfumo unaotumika kwenye TikTok.
Sehemu ya Search itahamishwa chini, kwenye nafasi iliyokuwa inatumiwa na icon ya Reels, huku Reels zikihamishwa kwenda kwenye nafasi ya Search. Instagram imesema mabadiliko haya yanalenga kutoa kipaumbele zaidi kwa Reels kutokana na umaarufu wake mkubwa.
Sehemu ya Notifications itabaki juu ya skrini kama ilivyokuwa awali, na haitaguswa na mabadiliko haya. Instagram imesema mabadiliko hayo yataanza kuonekana kwa watumiaji hatua kwa hatua duniani kote, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuboresha mwingiliano wa watumiaji na kuongeza muda wa matumizi ya programu hiyo.