
Kampuni ya Instagram imethibitisha kuwa ipo katika hatua za majaribio ya kipengele kipya kitakachowaruhusu watumiaji wake kushiriki tena (repost) machapisho ya wengine moja kwa moja kwenye wasifu wao.
Katika taarifa rasmi, Instagram ilieleza kuwa kipengele hiki kinachojaribiwa kwa sasa na watumiaji wachache kinalenga kurahisisha usambazaji wa maudhui, bila kuhitaji kutumia mbinu za ziada kama screenshot au programu za watu wa tatu.
Kipengele cha repost kitafanana kwa kiasi fulani na kile kinachopatikana kwenye mtandao wa X (zamani Twitter), ambapo watumiaji wanaweza kushiriki tena machapisho ya wengine kwa kubofya tu. Kwa mujibu wa Instagram, repost zitakuwa zinaonekana kwenye tab maalum katika wasifu wa mtumiaji, tofauti na machapisho ya kawaida.
Hatua hii imepokelewa kwa maoni tofauti mitandaoni. Baadhi ya watumiaji wamekaribisha mabadiliko hayo wakisema yataongeza ushirikiano na ueneaji wa maudhui, huku wengine wakihofia uwezekano wa maudhui ya watu kutumiwa vibaya bila ridhaa au muktadha sahihi.
Instagram, ambayo ni chini ya kampuni mama ya Meta, imesisitiza kuwa lengo la kipengele hicho ni kusaidia watumiaji kushirikiana zaidi na kuonyesha maudhui yanayowavutia au kuwagusa kwa urahisi.
Endapo majaribio yatafanikiwa, kipengele cha repost kinatarajiwa kuzinduliwa rasmi kwa watumiaji wote duniani katika miezi ijayo.