Kenya itawatumia wachezaji wake wa taekwondo wenye uzoefu katika mashindano ya dunia kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 21, ambayo yataandaliwa nchini kwa mara ya kwanza katika historia ya mchezo huo.
Mashindano hayo ya kimataifa yanatarajiwa kufanyika kuanzia Disemba 3 hadi 6 mwaka huu, katika Uwanja wa Kimataifa wa Kasarani, jijini Nairobi, na kuwavutia zaidi ya wachezaji 3,500 kutoka zaidi ya mataifa 150 duniani.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Taekwondo nchini, maandalizi ya mashindano hayo yako katika hatua za mwisho, huku tovuti rasmi ya mashindano hayo tayari ikizinduliwa, ikiwa ni jukwaa la kutoa taarifa kwa washiriki na mashabiki kutoka ndani na nje ya nchi.
Zaidi ya kuwa jukwaa la michezo, mashindano haya yanatazamiwa kuimarisha sekta ya utalii na kuchangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi, sambamba na kuwapa wachezaji wa Kenya nafasi ya kuonyesha vipaji vyao dhidi ya wapinzani wa kimataifa.
Timu ya taifa ya Kenya inatarajiwa kuingia kambini rasmi mwishoni mwa mwezi Novemba ili kujiandaa kikamilifu kwa mashindano hayo.