
Rap ya Kenya imewaka moto tena baada ya marapa Octopizzo na Kayvo KForce kujipata wakirushiana maneno makali kiasi cha karibu kuzichapa kwa makonde.
Chanzo cha mvutano huu kilikuwa diss track ya Kayvo, iliyolenga moja kwa moja kuhoji uhalali wa Octopizzo katika kiwanda cha hip hop. Baada ya Diss hiyo, wawili hao walikutana uso kwa uso, hali ikawa tete. Octopizzo alionekana kumwonya Kayvo akome, akimtaka aache kuingilia maisha yake ya muziki kwa kuachia βdiss tracks za kijingaβ na badala yake ajikite kuboresha sanaa yake.
Kayvo hakusita kujibu, akimtuhumu Octopizzo kwa kudhoofisha jina lake. Alidai kuwa kauli za rapa huyo kwenye Iko Nini Podcast, kwamba hatoki Kibera, zilimchafua hadharani. Octopizzo naye hakusalia kimya; alirudisha moto kwa kudai Kayvo amekuwa akijipendekeza kama mwana wa Kibera ilhali hajakulia wala kuishi humo. Kayvo alipuuza hoja hizo akisisitiza kwamba hazina mashiko.
Kauli hizo zilimkera zaidi Octopizzo, ambaye alimtaka Kayvo aonyeshe makazi yake Kibera kama anadai ni mwenyeji. Aidha, alimshutumu kwa kutumia jina la Kibera kwa manufaa binafsi.
Mzozo huo uliwafikisha pabaya kiasi cha kushikana mashati na kuanza kurushiana makonde, lakini hali hiyo ilidhibitiwa na watu wa karibu waliowaingilia kati.
Kwa kumbukumbu, wawili hao waliwahi kuwa marafiki na hata kuachia wimbo wa pamoja uitwao βVoice of Kiberaβ mwaka 2011, kabla ya nyota ya Octopizzo kungβaa na kupelekea tofauti za kimawazo na kimaisha.