
Rapa maarufu kutoka Marekani, Kodak Black, amepata heshima ya kipekee kwa kukabidhiwa Ufunguo wa Jiji la Pompano Beach (Key to the City) katika hafla maalum iliyofanyika Jumanne, Julai 8, 2025. Tukio hilo limeandaliwa kama njia ya kutambua mchango mkubwa wa msanii huyo kwa jamii ya mji alikozaliwa na kukulia – Pompano Beach, Florida.
Uongozi wa jiji hilo umetambua juhudi za Kodak Black, si tu kama msanii aliyefanikia katika muziki wa hip-hop, bali pia kwa moyo wake wa kujitolea kusaidia jamii kupitia miradi ya kijamii na misaada ya kifedha.
Kwa kipindi cha miaka kadhaa, Kodak Black ambaye jina lake halisi ni Bill K. Kapri amekuwa mstari wa mbele kusaidia vijana, shule, na familia zenye uhitaji. Amefadhili masomo ya wanafunzi kutoka familia zisizojiweza, kutoa misaada kwa waathirika wa majanga, na kusaidia programu zinazolenga kuzuia uhalifu na kukuza vipaji vya vijana mitaani.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kodak Black alitoa shukrani zake kwa viongozi wa jiji na jamii nzima kwa heshima hiyo kubwa.
“Najivunia kuwa sehemu ya Pompano Beach na nitaendelea kuwekeza kwa jamii yangu kwa kila njia niwezayo,” alisema rapa huyo.
Heshima ya kukabidhiwa Key to the City ni mojawapo ya heshima za juu kabisa ambazo jiji linaweza kumpa raia wake, na kwa Kodak Black, ni uthibitisho wa mafanikio yake si tu jukwaani, bali pia katika maisha ya kijamii.