
Wasanii wa kundi la Wadagliz kutoka nchini Kenya wamefanikiwa kusajili msemo wao maarufu wa Anguka Nayo ambao umebeba jina la wimbo wao kama chapa au nembo ya kibiashara.
Taarifa hiyo imethibitishwa na lebo ya muziki ya Hood Music kupitia ukurasa wake rasmi wa Instagram na kusema kuwa Wadagiliz kwa sasa ndiye wamiliki halisi wa jina hilo kwa mujibu wa sheria.
Lebo ambayo inasimamia kazi za Wadagiliz imetoa angalizo kwa atakayetumia nembo hiyo kwa shughuli za kibiashara bila ridhaa ya wasanii hao na uongozi wao huenda akachukulia hatua kali za kisheria ambayo itajumuisha kulipa faini.
Anguka Nayo ni moja kati ya ngoma iliyoitambulisha kikundi cha Wadagliz kwenye tasnia ya muziki nchini Kenya mwaka wa 2024 lakini pia imewafunguliwa milango ya mafanikio kutokana na shoo mbali mbali ambazo wamekuwa wakipewa mwaliko kutumbuiza. Mpaka sasa video ya wimbo wa Anguka Nayo ina zaidi ya watazamaji millioni 10 kwenye mtandao wa Youtube ndani ya kipindi cha miezi sita iliyopita.