
Kundi la muziki la Uingereza NSG limekanusha madai kuwa liliwavunjia heshima Wakenya usiku wa kuamkia Desemba 2022 wakiwa kwenye harakati za kutafuta chakula cha jioni.
Kupitia ukurasa wao wa Twitter NSG imedai kuwa mtu aliyekuwa kwenye video iliyosambaa mtandaoni hakuwa sehemu ya timu yao huku wakisema wanawaheshimu sana Wakenya kwa kuwa wanapata uungwaji mkubwa kwenye muziki wao kutoka Kenya.
Kundi hilo liliongeza kuwa watu walichukulia mtu alionekana kwenye video hiyo ni sehemu ya wafanyakazi wa NSG kwa sababu tu alikuwa na lafudhi ya Uingereza.
Kauli yao imekuja mara baada ya Mtengeneza maudhui wa Kenya Elodie Zone kupakia video kwenye mitando ya kijamii akidai kuwa mmoja wa wanachama wa NSG alimdhalalisha mhudumu wa Chicken inn jijini Nairobi alipokuwa anamhudumia kwa kumtupia matusi akisema anataka kuhudumiwa mara moja.
Elodie Zone alilaani kitendo hicho akisema ni dharau kwa wageni kuja Kenya na kuwavunjia heshima watu ambao wako katika maeneo yao ya kazi wakijaribu kujitafutia riziki.
Ikumbukwe kundi la NSG lenye makao yake nchini Uingereza lilifanya show yao usiku wa kuamkia leo katika uwanja wa Diamond Plaza, Nairobi.