
Mwanamuziki wa Kenya, Kush Tracy, amefunguka kuhusu maisha yake ya zamani kabla ya kuacha pombe, akieleza jinsi ulevi ulivyompeleka katika hali ya kupoteza mwelekeo wa maisha na muziki wake.
Akizungumza katika mahojiano na kipindi cha NTV Elevate, Kush Tracy alikiri kuwa hakuwahi kutumbuiza jukwaani akiwa akili timamu.
“Sikuwahi kuimba nikiwa sober. Nilihitaji kitu cha kunipa ujasiri, lakini kwa kweli ilikuwa ni njia ya kuficha matatizo,” alisema kwa dhati.
Mwanamuziki huyo pia alifichua kuwa ulevi ulimfikisha katika hali ya kufanya mambo ambayo hayakuwa sehemu ya tabia yake, ikiwa ni pamoja na kubusu wanaume asiowajua.
“Nilijikuta nikiwa katika hali ya kuchanganyikiwa, nikifanya mambo ya aibu kama kumbusu mwanaume nisiyemfahamu kabisa,” aliongeza.
Hata hivyo, Kush Tracy alisema kuwa alichukua hatua ya kubadilika na sasa ana miaka miwili tangu aache pombe. Alieleza kuwa bado anakumbana na watu wanaotaka kumrudisha katika maisha ya zamani, lakini ameweka msimamo wake wa kuendelea kubaki imara katika safari yake ya mabadiliko.
“Nilipata wokovu na nikakubali kuachana na maisha ya awali. Lakini baadhi ya watu wanajaribu kunirudisha kwenye ule uhalisia niliokuwa, jambo ambalo siwezi kukubali,” alisema kwa msisitizo.
Ushuhuda huo wa Kush Tracey, ambaye kwa sasa ameokoka,umeibua hisia mseto mitandaoni, huku mashabiki wengi wakimsifu kwa ujasiri wake wa kueleza hadharani changamoto alizopitia na uamuzi wake wa kubadilika.