LifeStyle

Linex Ahamasisha Wasanii Walioathirika Kisaikolojia Kuendelea na Muziki

Linex Ahamasisha Wasanii Walioathirika Kisaikolojia Kuendelea na Muziki

Msanii wa Bongo Fleva, Linex Sunday Mjeda, ametuma ujumbe kupitia InstaStory akiwashauri wasanii wanaokumbwa na changamoto za afya ya akili, hususan msongo wa mawazo, kurudi studio na kuendelea na kazi zao za sanaa.

Katika ujumbe wake, Linex alionesha kusikitishwa na hali ya baadhi ya wasanii kupotea kwenye muziki kutokana na matatizo ya kiakili. Alisisitiza kuwa kazi ya sanaa ni tiba na njia muhimu ya kupambana na changamoto za maisha, akihimiza kuwa kazi haidanganyi.

“Wanaopitia magonjwa ya akili kwenye muziki/sanaa, huwa mmefanyiwa makubwa yapi mpaka mpagawe na mshindwe kurudi studio? Em rudini studio, fanyeni kazi – kazi haisemagi uongo. Depression my mxiiiiiiiieww…,” alisema kupitia ujumbe wake uliojaa hisia Instagram.

Kauli ya msanii huyo imeibua maoni mseto kutoka kwa mashabiki na wadau wa sanaa, wengine wakiona ni wito wa kuhamasisha, huku wengine wakihisi kuwa masuala ya afya ya akili yanahitaji kuangaliwa kwa makini na kwa huruma zaidi.

Katika miaka ya karibuni, wasanii kadhaa kutoka ukanda wa Afrika Mashariki wamekuwa wakifunguka kuhusu changamoto za kiakili wanazopitia, huku mashabiki na wanaharakati wakizidi kutoa wito kwa jamii kuwa na uelewa zaidi kuhusu afya ya akili.

Ujumbe wa Linex umetafsiriwa na wengi kama wito kwa wasanii kuendelea kupambana na kutafuta uponyaji kupitia kazi zao za muziki na sanaa.