
Klabu ya Liverpool inatarajiwa kumtangaza rasmi beki wa kulia wa klabu ya Bayer Leverkusen, Jeremie Frimpong, ndani ya saa 24 zijazo baada ya mchezaji huyo kukamilisha vipimo vya afya.
Frimpong, raia wa Uholanzi mwenye asili ya Ghana, anakuja kama mbadala wa Trent Alexander-Arnold ambaye tayari ametangaza kuondoka Liverpool mwishoni mwa msimu huu. Liverpool wanaripotiwa kulipa ada ya pauni £29.5 milioni, ambayo ni sehemu ya kipengele cha kuachiliwa kilichopo kwenye mkataba wake na Leverkusen.
Frimpong alikuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya Leverkusen chini ya kocha Xabi Alonso, akisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Bundesliga bila kupoteza mchezo wowote msimu wa 2024/25. Ujio wake Anfield unatazamiwa kuimarisha safu ya ulinzi ya Liverpool kuelekea msimu mpya wa EPL.