
Prodyuza mahiri wa muziki nchini Tanzania, Lizer Classic, ameendelea kueleza hasira zake dhidi ya baadhi ya wasanii chipukizi (underground) ambao wamekuwa wakiripoti kazi za wasanii wakubwa kwenye YouTube kwa lengo la kujipatia umaarufu na fedha kupitia skendo hizo.
Kupitia Instagram, Lizer ametoa mfano wa kisa kilichomhusu msanii nyota Nandy, ambapo moja ya kazi zake iliripotiwa bila msingi, jambo ambalo limeonekana kama kikwazo kikubwa kwa juhudi za wasanii na maprodyuza wanaoweka muda na gharama kubwa katika kazi zao.
Ameeleza kuwa tabia hiyo ni ya kukatisha tamaa na inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa ukuaji wa muziki wa Tanzania kimataifa. Kwa mujibu wake, kitendo cha kuchukulia kwa wepesi kazi za wasanii wakubwa ni ukosefu wa heshima na nidhamu katika sanaa.
Lizer amewataka wasanii wote kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wale wanaojihusisha na tabia hiyo, akisema hatua hizo zitakuwa funzo kwa wengine na kusaidia kulinda kazi za wasanii wote nchini Tanzanzia.