
Mwanamuziki nguli kutoka Uganda, Maddox Ssematimba, amesisitiza umuhimu wa wasanii wa Uganda kuendeleza ubunifu na uhalisia wa muziki wa ndani badala ya kunakili mitindo kutoka mataifa mengine, hususan Nigeria.
Licha ya kutotoa nyimbo mpya kwa muda mrefu, Maddox bado anaheshimika kama nguzo muhimu ya muziki wa Uganda, akiwa maarufu kwa vibao vyake vya kihistoria kama “Nakatude” na “Namagembe”, ambavyo vinaendelea kupendwa na kusikika kote nchini Uganda hadi leo.
Katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni, Maddox alitoa wito kwa wasanii wa kizazi kipya kuwa na sauti ya kipekee na kuendeleza utambulisho wa muziki wa Uganda. Alieleza kuwa ubunifu na uhalisia wa kazi ndio humfanya msanii kudumu katika tasnia.
“Tuwe na muziki wetu wa kipekee. Tuache kunakili Wanaijeria. Ubunifu na uhalisia ndio hujenga msanii na kufanya kazi zake zidumu hata miaka mingi baada ya kutoka,” alisema Maddox.
Alitoa mfano wa wasanii kama John Blaq na Jose Chameleone, akiwapongeza kwa kuendeleza utambulisho wa muziki wa Uganda kupitia kazi zao zenye asili ya Kiafrika.
Aidha, Ssematimba alisisitiza umuhimu wa usimamizi bora kwa wasanii wanaotaka kupiga hatua kibiashara katika tasnia hiyo. Alieleza kuwa menejimenti bora ndiyo msingi wa mafanikio kwa msanii yeyote anayelenga kujijenga kitaaluma.
“Nadhani yote yanahusiana na menejimenti. Msanii akiamua kufanya muziki kibiashara, anahitaji kuwa na misingi imara. Menejimenti bora inaweza kumfikisha msanii mahali popote,” aliongeza.
Kauli za Maddox zimepokelewa kwa uzito katika tasnia ya burudani nchini Uganda, ambapo wengi wameona kama mwito wa kurejesha hadhi ya muziki wa asili ya Uganda katika soko la Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.