Entertainment

Mahakama Yakataa Dhamana kwa Ringtone Kufuatia Mashtaka ya Utapeli wa Ardhi ya Shilingi Milioni 50

Mahakama Yakataa Dhamana kwa Ringtone Kufuatia Mashtaka ya Utapeli wa Ardhi ya Shilingi Milioni 50

Mwimbaji maarufu wa muziki wa injili nchini Kenya, Alex Apoko, Maarufu Ringtone, amepata pigo kubwa hapo jana baada ya Mahakama ya Nairobi kukataa ombi lake la kuachiliwa kwa dhamana.

Ringtone na mshukiwa mwenzake Alfred Juma Ayora wanashtakiwa kwa kosa la kula njama ya kutapeli ardhi yenye thamani ya shilingi milioni hamsini, inayodaiwa kumilikiwa na Bi. Teresiah Adhiambo katika mtaa wa kifahari wa Karen, jijini Nairobi.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, wawili hao wanadaiwa kutoa madai kuwa wameishi katika ardhi hiyo kwa zaidi ya miaka ishirini na kwa hivyo wanastahili kupewa umiliki wa ardhi hiyo kwa mujibu wa sheria ya “adverse possession”, inayomruhusu mtu kumiliki  ardhi au mali isiyokuwa yake kisheria  endapo atakuwa ameimiliki kwa muda mrefu bila pingamizi kutoka kwa mmliki halali.

Hata hivyo, upande wa mashtaka unasema madai hayo ni ya kupangwa kwa lengo la kuipora ardhi hiyo kwa njia ya hila na nyaraka za uongo. Mahakama iliielezwa kuwa wamiliki halali wa ardhi hiyo hawajawahi kuondoka wala kuachia umiliki kwa washitakiwa.

Katika uamuzi wake, mahakama ilitaja sababu kadhaa za kukataa dhamana, ikiwemo uzito wa kosa, historia ya mshtakiwa kuhusishwa na kesi kama hizi hapo awali, na hatari ya kuingilia ushahidi au mashahidi.

Kumbuka, mwaka 2016, Ringtone alihusishwa na mgogoro wa nyumba ya kifahari katika mtaa wa Runda. Aidha, mwaka 2023, familia ya raia wa Sudan Kusini ilimshtaki kwa madai ya kuvamia mali yao huko Karen na kuharibu vitu vyao.

Ringtone, kwa upande wake, amekanusha mashtaka haya, akisema ni njama ya kumchafua hadharani na kumvunjia heshima kama mtu wa imani. Amekuwa akidai kuwa yeye ni mpangaji halali wa ardhi hiyo kwa muda mrefu.

Kwa sasa, Ringtone na mshukiwa mwenzake wataendelea kuzuiliwa rumande hadi kesi itakapoanza kusikilizwa rasmi. Mahakama imesisitiza kuwa mchakato wa haki utafuatwa kikamilifu, na uamuzi wa mwisho utategemea ushahidi wa pande zote mbili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *