
Makala ya nne ya mbio za marathoni za jiji la Nairobi yatafanyika kesho, Jumapili, huku zaidi ya washiriki 15,000 kutoka mataifa 75 wakitarajiwa kushiriki.
Kwa mujibu wa waandaaji, mbio hizo zitaanza na kumalizika katika uwanja wa Uhuru Park, jijini Nairobi, na zitaandaliwa hasa katika barabara ya Nairobi Expressway. Hii ni mara ya kwanza kwa sehemu kubwa ya marathoni hiyo kupita kwenye Expressway nzima, hatua inayolenga kuonyesha hadhi ya barabara hiyo mpya ya kisasa.
Kutokana na shughuli hiyo, wenye magari jijini Nairobi wanashauriwa kupanga safari zao kwa uangalifu na kutarajia msongamano mkubwa wa magari katika baadhi ya maeneo ya jiji. Barabara ya Nairobi Expressway itafungwa pande zote mbili kuanzia saa 10:00 usiku huu, kutoka eneo la James Gichuru hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), na itafunguliwa tena saa 3:00 asubuhi kesho.
Katika makala ya mwaka jana, Eliud Magut kutoka Kaptagat aliibuka mshindi katika mbio za wanaume za kilomita 42 kwa muda wa saa 2, dakika 9 na sekunde 47. Alimaliza mbele ya Josphat Bett na Emmanuel Sikuku walioshika nafasi ya pili na ya tatu mtawalia.
Kwa upande wa wanawake, Cynthia Jerotich aliibuka mshindi baada ya kukamilisha mbio hizo kwa muda wa saa 2, dakika 28 na sekunde 2. Lilian Chebii na Peris Jerono walifuatia katika nafasi ya pili na ya tatu.
Mwaka huu, jumla ya shilingi milioni 24 zimetengwa kama zawadi kwa washindi mbalimbali, huku shilingi milioni 11.4 zikitengwa kwa wanariadha 22 bora katika mbio za kilomita 42. Zawadi hizo zimevutia washiriki wa kiwango cha juu kutoka ndani na nje ya nchi, na mashindano yanatarajiwa kuwa ya ushindani mkubwa.
Waandaaji wamesema maandalizi yako tayari, na wamesisitiza kuwa usalama na afya ya washiriki na watazamaji ni kipaumbele kikuu katika marathoni ya mwaka huu.