Sports news

Malkia Strikers Yaendeleza Msururu wa Vichapo Katika Mashindano ya Dunia

Malkia Strikers Yaendeleza Msururu wa Vichapo Katika Mashindano ya Dunia

Timu ya taifa ya wanawake ya voliboli, Malkia Strikers, ilipata kichapo cha pili mfululizo katika mashindano ya voliboli ya dunia baada ya kushindwa na Poland seti tatu kwa moja kwenye mechi iliyopigwa jana jioni nchini Thailand. Hii ni mechi ya pili kwa Kenya kupoteza, baada ya kulazwa na Ujerumani katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa Jumamosi.

Mchezo dhidi ya Poland ulianza kwa changamoto kwa upande wa Kenya, ambapo waliangushwa kwa alama 25-17 katika seti ya kwanza. Hata hivyo, Malkia walirejea na kuonyesha matumaini katika seti ya pili, wakicheza kwa nidhamu na kuibuka kidedea kwa alama 25-15, hali iliyowapa mashabiki matumaini ya kurejea mchezoni.

Lakini matumaini hayo hayakudumu kwa muda mrefu, kwani Poland walichukua udhibiti wa seti ya tatu kwa ushindi wa 25-15, kisha wakaendelea kutawala mchezo katika seti ya nne na kuifunga Kenya kwa alama 25-14, hivyo kumaliza mchezo huo kwa ushindi wa seti 3–1.

Malkia Strikers sasa wanajiandaa kwa mtihani mwingine dhidi ya Vietnam katika mechi yao ya tatu, itakayopigwa siku ya Jumatano, tarehe 27 Agosti. Mechi hiyo inaonekana kuwa ya muhimu sana kwa Kenya, kwani ushindi unaweza kufufua matumaini yao katika mashindano haya ya kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *