
Msanii maarufu wa dancehall kutoka Jamaica, Spice, amezua gumzo baada ya kumtamkia hadharani mwanamuziki wa Kanada, Drake, kuwa ni “crush” wake wa muda mrefu. Tukio hilo lilijiri wakati wa onyesho lake la kusisimua katika tamasha la Wireless Festival, ambapo alikonga nyoyo za mashabiki kwa miondoko ya nguvu na burudani ya kiwango cha juu.
Spice, anayefahamika kama Queen of Dancehall, alichukua fursa hiyo kuonyesha mapenzi yake ya wazi kwa Drake kupitia remix ya kibabe ya wimbo wake maarufu One Dance. Katika mdundo huo uliopigwa kwa mtindo wa Karibea, Spice aliongeza ladha ya Jamaica kwa sauti na mahaba kwa kucheza kwa weledi, hali iliyowafanya mashabiki kulipuka kwa shangwe na kushangilia kwa nguvu.
Wakati akiimba na kucheza kwa miondoko ya kuvutia, Spice alisema, “Wacha niseme ukweli, nimekuwa na hisia kwa Drake kwa miaka”! Kauli hiyo ilitawala mitandao ya kijamii huku mashabiki wengi wakionekana kuvutiwa na ujasiri wake.
Tamasha la Wireless Festival ambalo hufanyika Uingereza, limeendelea kuwa jukwaa la kusisimua kwa wasanii wa kimataifa, na onyesho la Spice mwaka huu limeongeza moto kwa jinsi alivyochanganya muziki, mahaba, na ucheshi wa jukwaani, kwa mtindo wa kipekee wa Caribbean. Wengi sasa wanangojea kuona iwapo Drake atajibu hisia hizo au hata kufanya kazi ya pamoja na Malkia huyo wa Dancehall