Mama mzazi wa staa wa muziki wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, maarufu kama Mama Dangote, amesema wazi kuwa akifariki dunia, mwanawe atapata tabu sana kutokana na jinsi anavyomtegemea kihisia.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Mama Dangote ameeleza kwa hisia jinsi Diamond alivyorudi kutoka safarini na kuanza kudeka kama mtoto mdogo, hali inayomgusa sana kama mzazi. Amesema kuwa tabia hiyo inaonyesha namna mwanawe anavyompenda na kumthamini kama mama, licha ya kuwa mtu mzima mwenye umaarufu na mafanikio makubwa.
Mama Dangote, amesema Diamond anayejulikana kwa jina la utani Tom Kaka, amekuwa na uhusiano wa karibu sana naye kiasi kwamba kuondoka kwake kungemuumiza sana mwanawe huyo.
Mwanamama huyo ameongeza kwa utani kuwa “mtoto kwa mama hakui,” akimaanisha kuwa kwa mama, mtoto atasalia kuwa mtoto milele bila kujali umri au hadhi yake.
Ujumbe huo umevuta hisia za mashabiki wengi mtandaoni, wengi wakimpongeza Mama Dangote kwa maneno yake ya upendo na wengine wakigusia uhusiano wa kipekee uliopo kati yake na mwanamuziki huyo nyota wa Afrika Mashariki.