
Mashabiki wa mwanamuziki Kanye West wamelalamikia vikali onyesho lake lililofanyika mwishoni mwa wiki jijini Shanghai, wakimtuhumu kwa kuwasaliti na kudai warejeshewe pesa zao.
Kwa mujibu wa mashuhuda waliokuwepo kwenye tamasha hilo, Kanye alichelewa kuingia jukwaani kwa zaidi ya dakika 45 na alipoanza kutumbuiza, alionekana kulip-synch kwa sehemu kubwa ya onyesho hilo badala ya kuimba moja kwa moja.
Tukio hilo liliwakasirisha mashabiki waliokuwa wamelipia tiketi kwa matarajio ya kumuona msanii huyo kwa ubora wake wa kawaida. Baadhi yao walionekana wakipaza sauti kwa pamoja wakisema “refund! refund!” wakiashiria kutoridhishwa kwao na maonesho hayo.
Hadi sasa, Kanye West bado hajatoa tamko lolote rasmi kuhusu tukio hilo ambalo limezua mjadala mkali mitandaoni, huku wengine wakisema hali hiyo ni mwendelezo wa tabia zisizoeleweka kutoka kwa rapa huyo ambaye amekumbwa na migogoro mingi ya kipekee miaka ya hivi karibuni.