
Msanii nyota wa Kenya, Akothee, amezua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutoa kauli kali iliyotafsiriwa kama dharau kwa fundi aliyemtengenezea meza.
Kauli yake kwamba meza hiyo “inafanana na jeneza”, imechukuliwa na mashabiki kama ya kudhalilisha na kukosa heshima kwa mafundi wanaojituma kujitafutia riziki. Mashabiki waliitaja kauli hiyo kuwa ya kuumiza na kukosa utu, wakimtaka msanii huyo kuheshimu bidii ya mafundi wanaojituma licha ya changamoto.
“Hata kama hukupenda kazi, si lazima kumdhalilisha mtu. Huo ni ukatili,” aliandika shabiki mmoja.
Wengine walimtaka Akothee kutumia umaarufu wake kuhamasisha heshima kwa watoa huduma wa kawaida badala ya kuwavunjia hadhi hadharani. Pia, walihimiza mawasiliano ya moja kwa moja na ya staha kama njia bora ya kushughulikia changamoto za kibiashara.
“Umaarufu haumpi mtu ruhusa ya kumshusha mwingine hadharani. Wafanyakazi wa mikono wanastahili heshima pia,” aliongeza mwingine
Hadi sasa, Akothee hajatoa tamko lingine zaidi ya kauli yake ya TikTok, huku mjadala ukiendelea kushika kasi mitandaoni na wengi wakimtaka azingatie lugha na heshima anapotoa mrejesho kwa umma.
Mzozo huo ulianza baada ya fundi seremala kumuanika Akothee kwenye mitandao ya kijamii akidai kuwa hajalipwa salio la kazi yake, licha ya kumkabidhi meza aliyokuwa ameagiza. Katika kujibu kupitia TikTok Live, Akothee alidai tayari alimlipa fundi huyo asilimia 80 ya malipo lakini kazi aliyopokea haikukidhi matarajio yake.
“Nilimlipa 80%, lakini kazi si ya kiwango nilichotaka. Aichukue tu, hiyo meza inafanana na jeneza,” alisema Akothee mbele ya mashabiki wake mtandaoni.