
Mashabiki wa muziki Afrika Mashariki wameonyesha shauku kubwa ya kutaka msanii wa WCB Zuchu kutumbuiza kwenye ufunguzi wa Kombe la Dunia 2026, baada ya kuandika historia usiku wa kuamkia leo katika Siku ya Yanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Katika onyesho hilo lililohudhuriwa na zaidi ya mashabiki elfu 60, Zuchu alidhihirisha ubunifu wa kimataifa kwa mtindo wa kipekee wa kuingia jukwaani. Msanii huyo alifika uwanjani ndani ya chombo kilichofanana na ua kubwa, ambacho baadaye kilifunguka taratibu kama ua linalochanua, na Zuchu akaibuka kutoka ndani yake huku akiibua shamrashamra za burudani.
Mbali na hilo, aliwashangaza mashabiki kwa kuingia na kundi kubwa la madansa zaidi ya 200, hali iliyoongeza hamasa na kuifanya show yake kuzungumziwa kote mitandaoni. Zuchu alisema kuwa kiwango cha ubunifu kilichoonyeshwa hakijawahi kutokea kwenye historia ya shoo kubwa za uwanjani Tanzania.
Hali hiyo imezua mjadala mitandaoni, wengi wakimpongeza kwa hatua kubwa ya kuvuka mipaka ya burudani ya ndani na kuonyesha kwamba wasanii wa Afrika Mashariki wanaweza kushindana kimataifa. Baadhi ya mashabiki wameenda mbali zaidi wakimtaka Zuchu aorodheshwe miongoni mwa wasanii watakaopamba ufunguzi wa FIFA World Cup 2026, wakisema ubunifu na hadhi yake sasa inatosha kushindana na wakali wa dunia.