
Mwanamuziki kutoka Tanzania Zuchu amefutilia mbali matamasha yake ambayo yalikuwa yamepangwa kufanyika jijini Nairobi na Eldoret mwezi huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kampuni ya Trueblaq Limited na Jabali entertainment, matamasha hayo yamepangwa kufanyika mwaka ujao wikendi ya Pasaka.
“Kutokana na mazingira yaliyo nje ya uwezo wetu, tunasikitika kukujulisha kwamba vybez connect events iliyopanga kufanyika jijini Nairobi na Eldoret tukishirikiana na Zuchu pamoja na wasanii wengine wa Kenya haitaendelea kama ilivyopangwa.”, Ilisomeka taarifa hiyo
Matamasha ambayo yalikuwa yafanyike tarehe 10 na 11 Desemba 2022, sasa yatafanyika tarehe 8 na 9 Aprili 2023.
Waandaaji matamasha hayo wameomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza kwa mashabiki huku wakiwahakikishia wale ambao tayari walikuwa wamenunua tiketi wataweza kuzitumia tiketi hizo kwa ajili ya tamasha la Pasaka lililopangwa upya.
Hata hivyo wamesema pesa zitarejeshwa kwa wale ambao hawatafanikiwa kuhudhuria tamasha la Vybez Connect Events mwaka ujao.