
Msanii maarufu wa muziki wa Bongo Fleva, Mbwana Yusuf Kilungi maarufu Mbosso, ameripotiwa kupata jeraha kwenye mguu wake wa kulia wakati wa shughuli za utayarishaji wa kazi yake mpya ya muziki.
Tukio hilo lilitokea akiwa location akirekodi video, ambapo inadaiwa alidondoka ghafla baharini katika harakati za kuhakikisha mashabiki wake wanapata burudani ya kiwango cha juu. Ingawa haijafahamika ukubwa wa jeraha hilo, watu wa karibu na msanii huyo wamesema kuwa hali yake si ya kutia wasiwasi na anaendelea kupata matibabu.
Mashabiki wake wameonyesha wasiwasi kupitia mitandao ya kijamii, huku wengi wakimtumia jumbe za kumtakia afueni ya haraka.
Mbosso, anayejulikana kwa sauti yake ya kipekee na vibao kama Hodari na Fall, amekuwa akijiandaa na miradi mipya ya muziki, na tukio hili limekuja wakati mashabiki wakingoja kwa hamu kazi yake mpya.