
Mzozo kati ya Diamond Platnumz na msanii wake wa zamani Mbosso umeendelea kuchukua sura mpya baada ya wawili hao kufichua mambo ya ndani ya Label ya WCB Wasafi.
Baada ya Diamond kudai kuwa ameandika nyimbo nyingi za Mbosso na kumkopesha zaidi ya shilingi milioni 323 ambazo hakulipwa, Mbosso naye amejibu kwa kueleza kuwa yeye pia amekuwa akishiriki kuandika nyimbo za Diamond, ingawa hataki kuzitaja. Amesema tangu enzi zake akiwa Yamoto Band, Diamond alikuwa akimuita nyumbani kwake au studio kushiriki katika kazi hizo.
Kupitia Instastories, Mbosso amekanusha madai kwamba anamwonea wivu Diamond, akibainisha kuwa kuna watu wa kati wanaojaribu kuwapandikizia uhasama. Amesema wazi kuwa huenda Diamond alikuwa na jambo moyoni kwa muda mrefu na sasa ameona wakati umefika wa kulitoa hadharani. Hata hivyo, licha ya mkanganyiko huo, Mbosso amesema ataendelea kumheshimu Diamond kwa mchango wake mkubwa katika maisha yake ya muziki.
Kwa upande wake, Diamond amesisitiza kuwa Mbosso aliachwa na deni kubwa alipoondoka WCB, lakini aliamua kumsamehe bila malipo yoyote. Aidha, Diamond amedai kuwa wakati Rayvanny anaondoka WCB, Mbosso alimshawishi asifanye kazi naye, akimpinga kushirikiana naye kwenye nyimbo. Hata hivyo, Diamond amesema alikataa kuingiwa na chuki, akisisitiza kuwa kuondoka kwa msanii kwenye Label hakupaswi kuwa chanzo cha ugomvi.