
Mchekeshaji maarufu wa TikTok, Zakaria Kariuki, anayefahamika kwa jina la kisanii kama Mr. KK Mwenyewe, amefariki dunia akiwa anapokea matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kiambu (Kiambu Level 5 Hospital).
Taarifa za kifo chake zimetangazwa na rafiki yake wa karibu na mchekeshaji mwenzake, Kafengo, ambaye alielezea masikitiko yake kwa kumpoteza msanii aliyekuwa akileta furaha kwa mamilioni ya watu kupitia mitandao ya kijamii.
Mr. KK alipata umaarufu mkubwa baada ya video zake za kuigiza sauti na tabia za aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kusambaa sana kwenye mitandao ya kijamii, hususan TikTok. Uwezo wake wa kipekee wa kuigiza na kutumia ucheshi kuibua mijadala ya kijamii ulimfanya kupendwa na watu wa rika zote.
Kifo chake kimeibua majonzi makubwa miongoni mwa mashabiki wake, ambao wengi wao wameeleza kushtushwa na taarifa hizo, huku wakikumbuka mchango wake katika tasnia ya burudani.
Mpaka sasa, familia haijatoa taarifa rasmi kuhusu chanzo kamili cha kifo chake, huku mashabiki na wenzake katika sekta ya burudani wakiendelea kuomboleza.