Mwanamama Esther Musila amefunguka na kueleza sababu iliyowafanya yeye na mume wake, mwimbaji wa muziki wa injili Guardian Angel, kuamua kutumia maneno ya “for richer” pekee katika viapo vyao vya ndoa, na kuacha kipengele cha “for poorer” ambacho huonekana mara nyingi katika viapo vya kawaida vya ndoa.
Kupitia mitandao yake ya kijamii, Musila amesema waliamua kufanya hivyo kwa makusudi kwa sababu hawakutaka kutamka au kuingiza maneno yanayohusu umasikini au magumu katika ndoa yao, akisema kuwa maneno yana nguvu na yanaweza kuathiri mwelekeo wa maisha ya ndoa.
Esther Musila ameongeza kuwa uamuzi huo haukumaanisha kupuuza changamoto za maisha, bali ni kuchagua kuanza ndoa yao kwa matumaini, imani na malengo mema, huku wakimtegemea Mungu kuwaongoza katika kila hatua.
Kauli ya mwanamama huyo ambaye ndoa yake imepitia misusuko ya kupingwa na walimwengu, inakuja wakati anasherekea miaka minne ya ndoa yao na miaka sita ya kuwa pamoja tangu waanze uchumba wao.