
Mozilla imetangaza kuwa itasitisha huduma ya Pocket, programu ya kuhifadhi links, video na kurasa kwa kusoma baadaye, kuanzia Julai 8, 2025. App hii imekuwa maarufu miongoni mwa wapenzi wa habari na makala mtandaoni.
Kampuni hiyo imesema imeamua kufunga Pocket ili kuelekeza nguvu zaidi kwenye kuboresha kivinjari chake cha Firefox. Watumiaji wote wataarifiwa mapema na kupewa fursa ya kuhifadhi au kuhamisha maudhui yao kabla ya kufungwa kwa huduma hiyo.
Pocket ilianzishwa mwaka 2007 na kununuliwa na Mozilla mwaka 2017, na imekuwa muhimu kwa wanaopenda kusoma offline. Mozilla imeahidi kutoa msaada kwa watumiaji katika kipindi hiki cha mpito.
Hatua hii imepokelewa kwa hisia mchanganyiko, huku baadhi ya watumiaji wakieleza masikitiko yao mitandaoni, wakisema Pocket ilikuwa suluhisho bora kwa kusoma bila usumbufu. Wengine wamependekeza Mozilla kuifanya Pocket kuwa sehemu ya Firefox badala ya kuifunga kabisa.