Entertainment

Mr. Seed Afunguka kwa Uchungu: “Polisi Sio Marafiki Zetu”

Mr. Seed Afunguka kwa Uchungu: “Polisi Sio Marafiki Zetu”

Msanii wa muziki nchini Kenya, Mr. Seed, ameungana na Wakenya wanaomwombea Boniface Kariuki, kijana aliyepigwa risasi na polisi na ambaye kwa sasa yuko ICU, kwa kutoa ujumbe mzito wa majonzi na hasira kupitia mitandao ya kijamii.

Katika ujumbe wake wa wazi na wa kugusa hisia, Mr. Seed alisema kuwa hali ya usalama nchini inamfanya kujiuliza kama kweli polisi bado wanaweza kuaminika kama walinzi wa raia. Alieleza kuwa tukio hilo limemvunja moyo kiasi cha kufikiria kuwafundisha watoto wake kuwa polisi si marafiki, bali chanzo cha hofu kwa wananchi.

“Nahisi kama ni lazima nifundishe watoto wangu kuwa polisi si marafiki zetu, si ndugu wala dada zetu… wanatuua na kutufanya maisha kuwa magumu,” aliandika kwa uchungu.

Akiwa amejaa hasira na maumivu, Mr Seed aliongeza kauli kali ya kulaani ukatili wa polisi akimalizia ujumbe wake kwa maneno: “F** the popo!!”*

Kauli hiyo, licha ya kuwa na hisia kali, imezua mjadala mkubwa mtandaoni, ambapo baadhi ya wananchi walionyesha kuungana naye kwa maumivu yanayotokana na ukatili wa maafisa wa usalama, huku wengine wakihimiza matumizi ya lugha ya staha kutokana na nafasi yake kama msanii.

Mr. Seed ni miongoni mwa wasanii kadhaa waliotoa maoni yao kufuatia tukio la kupigwa risasi kwa Boniface, pamoja na Eric Omondi ambaye ametangaza kampeni ya kuvaa barakoa Ijumaa hii kama njia ya kumbukumbu na mshikamano kwa waathiriwa wa ukatili wa polisi.

Wito wa haki kwa Boniface Kariuki unaendelea kushika kasi, huku mashirika ya haki za binadamu yakitaka uchunguzi wa haraka na hatua kali kuchukuliwa dhidi ya waliohusika.

Huku hasira na huzuni zikiendelea kutanda nchini, sauti za wanamuziki na wasanii zinazidi kuwa sauti za wananchi, wakitaka mabadiliko ya kweli katika mfumo wa usalama wa taifa.