Msanii kutoka nchini Kenya, Dyana Cods, ameweka wazi idadi ya nyimbo zitakazopatikana kwenye albamu yake mpya inayotarajiwa kuingia sokoni hivi karibuni.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Dyana amewajulisha mashabiki wake kuhusu ujio wa albamu hiyo, akisema kuwa itakuwa na ngoma 16 za moto, huku akimalizia chapisho lake kwa hashtag #GhettoGirl, ikionekana kuwa huenda ndilo jina la albamu hiyo.
Ingawa hajafichua majina ya nyimbo hizo wala wasanii aliowashirikisha, Dyana amewataka mashabiki wake kukaa mkao wa kula kuipokea rasmi albamu hiyo ambayo inaashiria hatua mpya katika safari yake ya muziki.
Kwa mujibu wa rekodi zilizopo, Dyana Cods tayari ana albamu kadhaa zilizotolewa miaka ya nyuma zikiwemo Late Night Kneeler (2019), Thank Me Later (2022), River Lake Nilote (2023), na Rong Manners (2024).
Albamu yake mpya itakuwa ya tano katika msururu wa kazi zake, ikionyesha mwendelezo wa ubunifu na ukuaji wake katika tasnia ya muziki nchini Kenya.