
Mwanamuziki maarufu wa Kenya, Jovial, ameweka wazi safari yake ya ujauzito ambayo anaiita kuwa mojawapo ya vipindi vigumu zaidi katika maisha yake ya hivi karibuni.
Kupitia ujumbe aliouweka kwenye mitandao ya kijamii, Jovial ameeleza jinsi hali ya ujauzito ilivyomchosha na kumrudisha nyuma kiafya na kisaikolojia. Amesema wazi kuwa trimester ya kwanza (miezi mitatu ya mwanzo) ndiyo ilikuwa ngumu zaidi kwake, akifichua kuwa kulikuwa na wakati alikaa wiki nzima bila kuoga kutokana na uchovu na mabadiliko ya mwili.
“Siwezi kudanganya, katika trimester yangu ya kwanza, niliishi wiki nzima bila hata kuoga. Nilikuwa nimechoka, sina hamu ya kitu chochote, mwili ulikuwa umelegea na akili ilikuwa mbali kabisa,” Aliandika Jovial
Jovial, ambaye anajulikana kwa vibao kama Such Kinda Love na Jeraha, amesema alikuwa akipitia hisia kali ambazo zilimfanya ajihisi mnyonge na wakati mwingine kujiuliza kama hali hiyo ni ya kawaida kwa kila mwanamke mjamzito.
Mashabiki wake wengi waliitikia kwa huruma na kumpa moyo, wakimtakia kila la heri katika safari yake ya uzazi. Wengine pia wamemsifu kwa kuwa mkweli na kueleza hadharani jambo ambalo wanawake wengi huwa wanapitia lakini huogopa kulizungumza.
Jovial hajataja muda kamili wa kujifungua, lakini mashabiki wake wanaonekana kuwa na shauku ya kumuona mama mpya akiibuka tena na nguvu mpya katika muziki.