
Msanii maarufu wa muziki wa Kenya, Jovial, ametangaza rasmi kuwa anatarajia mtoto na mchumba wake, Mike, kupitia wimbo wake mpya unaoitwa “Chibaby”, ambao tayari umeanza kuvuma mitandaoni.
Taarifa hiyo ya kufurahisha ilifichuliwa kupitia video ya kipekee aliyopakia kwenye ukurasa wake wa Instagram, ambapo alionekana akiwa mwenye furaha tele, akicheza na kuimba kwa bashasha huku akionyesha wazi tumbo la ujauzito. Video hiyo iliwagusa mashabiki wake wengi, ambao walimiminika kwenye sehemu ya maoni kumpa pongezi na salamu za heri kwa hatua hiyo kubwa ya maisha.
Katika wimbo wa Chibaby aliyomshirikisha msanii wa Biongofleva Ibraah, Jovial anasifia mapenzi ya dhati, amani ya ndoa, na furaha ya kutarajia mtoto. Mashairi ya wimbo huo yanadhihirisha hisia za shukrani na matumaini, huku akimtaja mchumba wake kama mshirika wa kwelin a mtoto wao kama zawadi ya maisha.
Mtoto anayetarajiwa atakuwa wa kwanza kwa Jovial na Mike, na hatua hii imepokelewa kama mwanzo mpya katika safari yao ya kifamilia. Licha ya kuwa mmoja wa waimbaji walioweka alama katika muziki wa kisasa nchini Kenya, Jovial ameonyesha kuwa maisha ya wasanii hayahusu kazi pekee, bali pia kupanda na kushuka kwa maisha ya kawaida, ikiwemo uzazi na ujenzi wa familia.
Mashabiki wanasubiri kwa hamu zaidi taarifa kutoka kwa msanii huyo kuhusu ujio wa mtoto na mipango yake ya baadaye, huku wengine wakimtaja kama mfano wa kuigwa kwa usawa wa kazi na maisha binafsi.