
Msanii wa nyimbo za Injili, Alex Apoko almaarufu Ringtone, aliachiliwa kwa dhamana ya Shilingi milioni 3 au kwa njia mbadala ya bondi ya Shilingi milioni 1, katika kesi inayomkabili ya kula njama ya kutapeli ardhi.
Ringtone alifikishwa katika Mahakama ya Milimani siku ya Alhamisi, pamoja na mshukiwa mwenzake Alfred Juma Ayora, wakikabiliwa na shtaka la kula njama ya kumlaghai mwanamke mmoja kipande cha ardhi chenye thamani ya Shilingi milioni 50.
Kwa mujibu wa mashtaka, wawili hao wanadaiwa kupanga njama ya kumtapeli Teresiah Adhiambo kipande cha ardhi kilichoko eneo la Karen, Nairobi, chenye nambari ya usajili NAIROBI/BLOCK 99/142 na ukubwa wa takribani ekari 0.1908.
Upande wa mashtaka unadai kuwa mnamo au kabla ya Februari 28, 2023, Ringtone na mwenzake walijifanya kuwa wamiliki halali wa ardhi hiyo kwa madai kuwa wameishi humo kwa kipindi cha miaka 20 kwa mujibu wa umiliki wa muda mrefu (adverse possession), jambo ambalo walijua si la kweli.
Kesi hiyo imepangiwa kusikizwa katika tarehe ijayo huku washukiwa wakiendelea kupewa masharti ya dhamana walizopewa na mahakama.