Msanii wa muziki wa injili nchini Kenya, Betty Bayo, ameaga dunia akiwa anapokea matibabu katika Hospitali ya Kenyatta, Nairobi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na watu wa karibu naye, Betty Bayo alikuwa akipokea matibabu kwa muda kabla ya hali yake kuzorota na kufariki dunia akiwa hospitalini.
Betty Bayo alijulikana kwa sauti yake yenye mvuto na nyimbo zilizogusa maisha ya wengi, nyimbo zake maarufu Maneno na Siyabonga, zilimpatia umaarufu mkubwa katika muziki wa injili nchini Kenya.
Mbali na taaluma yake ya muziki, marehemu pia alikuwa mke wa zamani wa mchungaji Victor Kanyari, na wawili hao walikuwa wamejulikana sana kutokana na ndoa yao iliyokuwa ikifuatiliwa kwa karibu na vyombo vya habari.
Habari za kifo chake zimetikisa tasnia ya muziki wa injili na kuibua majonzi miongoni mwa mashabiki na viongozi wa dini huku wengi wakituma salamu za rambirambi kwa familia yake.