
Mwanamuziki kutoka Uganda, Bruno K, ameanzisha kampeni ya kuchangisha fedha kusaidia mazishi ya msanii wa injili wa Rwanda, Gogo Gloriose, aliyefariki dunia nchini Uganda tarehe 4 Septemba baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Kupitia TikTok Live akiwa na meneja wa marehemu, Bruno K ameeleza kuwa kuna uhitaji wa dharura wa msaada wa kifedha ili kulipa bili ya hospitali na kuandaa usafirishaji wa mwili wa Gogo kurudi Rwanda kwa mazishi. Amesisitiza kuwa Gogo hakuja Uganda kwa shughuli za kibiashara bali alikuwa akihudumu, hivyo ni jukumu la mashabiki na makanisa aliyowahi kuhudumu kushirikiana kumpa heshima ya mwisho.
Hata hivyo amebainisha pia kuwa mchango huo unahitajika kwa ajili ya kulipa bili ya hospitali, kununua jeneza na kugharamia gharama za usafirishaji wa mwili wake kuelekea Rwanda.
Marehemu, kwa jina halisi Gloriose Musabyimanna, alikuwa amesafiri Uganda kuhudhuria ibada ya injili alipougua ghafla na kulazwa hospitalini Kyengera ambako alifariki dunia.