 
									Tasnia ya muziki nchini Uganda imo kwenye majonzi kufuatia kifo cha mwanamuziki Olisha M, aliyeripotiwa kufariki jana jioni wakati wa kujifungua katika hospitali moja maarufu jijini Kampala.
Olisha M, anayejulikana kwa vibao vyake kama Katambala, Super Love, na Gwenjagala, alikuwa mmoja wa wanamuziki chipukizi waliokuwa wakifanya vyema kwenye muziki wa kizazi kipya nchini humo. Habari za kifo chake zimeutikisa ulimwengu wa burudani na kuwahuzunisha mashabiki wake ndani na nje ya Uganda.
Mwanamuziki huyo, ambaye mwaka jana alifanikisha sherehe ya kumtambulisha rasmi mchumba wake katika hafla iliyovutia umma, aliripotiwa kuwa katika hali nzuri ya kiafya kabla ya tukio hilo la kusikitisha kutokea.
Tangu taarifa za kifo chake kutangazwa, mitandao ya kijamii imefurika jumbe za rambirambi kutoka kwa mashabiki, wasanii wenzake, na wadau wa muziki waliomkumbuka kwa sauti yake na mchango wake katika sanaa.
 
								 
             
             
                             
                             
                             
                             
                             
                             
                            