Entertainment

Mtangazaji Mgenge Azindua Kipindi Kipya cha HipHop

Mtangazaji Mgenge Azindua Kipindi Kipya cha HipHop

Mtangazaji maarufu wa redio, Mgenge, kwa kushirikiana na Mountainline Production ametangaza kuzindua kipindi kipya cha No Pen No Pad kinachojikita katika muziki wa HipHop nchini Tanzania. Kipindi hiki kinatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa na kuibua sura mpya katika tasnia ya Rap.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mgenge ameeleza kuwa muziki wa Rap umepoteza mvuto wake wa awali hapa nchini ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Kupitia kipindi cha No Pen No Pad, atatoa nafasi kwa wasanii wa Rap kuonyesha uwezo wao kupitia mashindano ya freestyle, beat making, na mazungumzo yenye tija yanayogusa utamaduni wa HipHop.

“Muziki wa Rap kwasasa hapa Tanzania umepungua mvuto kulinganisha na miaka ya nyuma, hivyo kupitia No Pen No Pad tutaleta sura mpya ambayo itakuwa ni mabadiliko ya kweli kwa wapenzi wa HipHop,” alisema Mgenge.

Kipindi hicho kitajumuisha vipindi vya “Freestyle, Beats & Daily Bars” pamoja na mazungumzo ya kina kuhusu utamaduni wa HipHop. Wapenzi wa muziki huo watakuwa na nafasi ya kufuatilia kipindi hicho kupitia YouTube kwenye channel ya Mountainline Studios.

Mgenge ameitaja No Pen No Pad kuwa jukwaa la kipekee litakalowawezesha wasanii wa HipHop kuonyesha ubunifu wao bila kuhitaji maandishi au vifaa vya kawaida vya kuandika, hivyo kuhimiza ubunifu wa papo kwa papo.

Kipindi kipya cha No Pen No Pad kinatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni na kinatarajiwa kuvutia hadhira kubwa kutoka kwa wapenzi wa HipHop hapa Tanzania na hata kwingineko.