Gossip

Mwanamume wa Tanzania Aliyedai Kurogwa kwa Kuiba Mbuzi Akiri Kuigiza Tukio Lote

Mwanamume wa Tanzania Aliyedai Kurogwa kwa Kuiba Mbuzi Akiri Kuigiza Tukio Lote

Mwanamume mmoja kutoka Tanzania ambaye hivi majuzi alivuma mitandaoni kwa kudai kuwa alirogwa na kuanza kutoa sauti za wanyama baada ya kuiba mbuzi, sasa amefichua kuwa tukio hilo lote lilikuwa la kuigiza.

Akizungumza katika mahojiano maalum na mtangazaji maarufu wa Kenya, Oga Obinna, mwanamume huyo alikiri kuwa alidanganya polisi na kuigiza sauti za mbuzi na mbwa kwa makusudi ili apate huruma na msaada wa nauli ya kuja Nairobi.

Katika video iliyosambaa sana mtandaoni, mwanamume huyo alionekana akitoa sauti kama za mbuzi na mbwa, hali iliyozua mjadala mkubwa huku baadhi ya watu wakiamini kuwa alikuwa ameathiriwa na uchawi baada ya kuiba mbuzi.

Hata hivyo, katika mahojiano hayo, alifichua kuwa hakurogwa na wala hakuhusishwa na wizi wa mifugo. Aliongeza kuwa kupitia huruma ya watu, alipata fedha za kutosha kumsafirisha hadi jijini Nairobi.

“Niliamua kuigiza ili nipate msaada. Nilijua watu wangenihurumia wakifikiri nimerogwa,” alisema.

Kauli yake imezua hisia mseto mitandaoni, baadhi wakimsifu kwa ujasiri wa kusema ukweli huku wengine wakimlaumu kwa kudanganya umma. Wengine wanahisi kuwa kitendo chake kinapotosha na kudhalilisha watu wanaopitia matatizo halisi ya afya ya akili au mateso ya kweli.

Hadi sasa, mamlaka kutoka Tanzania na Kenya bado hazijatoa taarifa rasmi kuhusu tukio hilo na kukiri kwake.