
Aliyekuwa msanii wa kikundi cha muziki wa Gengetone Sailors Gang, aitwaye Shalikido, ameomba msaada kutoka kwa Wakenya pamoja na mchekeshaji maarufu Eric Omondi ili kuisaidia familia yake.
Msanii huyo amesema licha ya kujaribu shughuli mbalimbali za kujikimu, bado anakumbana na changamoto kubwa za kifedha na ameshindwa kupata kipato cha kutosha kuendesha maisha ya kila siku.
Kwa mujibu wa Shalikido, hali ya muziki imekuwa ngumu kwa wasanii wengi wa kizazi kipya, hasa baada ya kupungua kwa fursa za maonyesho na changamoto za kimasoko. Ameeleza kuwa hatua ya kuomba msaada ni ya mwisho baada ya juhudi zake binafsi kutofanikisha maisha bora kwa familia yake.
Wito wake umewagusa mashabiki na wadau wa burudani, huku mjadala ukiibuka kuhusu hali ya wasanii wa Gengetone waliowahi kutamba lakini sasa wanakabiliwa na hali ngumu za kiuchumi.