Entertainment

Nandy Afunguka Sababu za Kukosekana kwa Video ya “Tonge Nyama”

Nandy Afunguka Sababu za Kukosekana kwa Video ya “Tonge Nyama”

Staa wa muziki kutoka Tanzania, Nandy, ametangaza rasmi kuwa hakutakuwa na video ya wimbo wake mpya alioufanya kwa ushirikiano na msanii Marioo, unaoitwa “Tonge Nyama.”

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Nandy amefafanua kwamba mashabiki wengi wamekuwa wakimuuliza kuhusu video ya wimbo huo na nafasi ya Marioo katika promosheni yake. Amebainisha kuwa wimbo huo kwa sasa unakabiliwa na hitilafu za kisheria, jambo lililosababisha uamuzi wa kutokutengeneza video.

Nandy pia ametoa shukrani kwa mashabiki waliouunga mkono wimbo huo kupitia changamoto mitandaoni, wanablogu, vyombo vya habari na vilabu vya usiku.

Hitmaker huyo wa Sugar, amesisitiza kuwa licha ya changamoto hizo, mashabiki wanaweza kuendelea kufurahia “Tonge Nyama” kupitia majukwaa mengine ya kidijitali na kwenye vilabu.

Msanii huyo amehitimisha waraka wake kwa kuwaahidi mashabiki wake miradi mipya, ikiwemo albamu mpya ambayo amesema ipo mbioni kuzinduliwa.

Nandy, amejikuta kwenye mgogoro na kijana anayejiita Mr Tonge Nyama, ambaye amedai kuwa jina lake limetumika na Nandy bila ridhaa yake katika wimbo mpya wa msanii huyo. Mr Tonge Nyama anataka alipwe fidia ya Shilingi Milioni 200 za Kitanzania, akisema jina hilo limetumiwa kwa manufaa ya kibiashara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *