Entertainment

Nandy Athibitisha Albamu Mpya Kutoka Mwezi Novemba

Nandy Athibitisha Albamu Mpya Kutoka Mwezi Novemba

Malkia wa muziki wa Bongo Fleva, Nandy,amefunguka kwa mashabiki wake kuhusu kusubiriwa kwa albamu yake mpya, akieleza kuwa itaachiwa rasmi mwezi Novemba mwaka huu.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mkali huyo wa ngoma ya “Sugar” aliwatuliza mashabiki waliokuwa wakihoji ni lini albamu hiyo itatoka, huku akifafanua kuwa kuchelewa huko kumesababishwa na sababu za msingi, ikiwa ni pamoja na kukamilisha kolabo zilizobaki na maandalizi ya mwisho ya albamu yenyewe.

“Mashabiki zangu, comments zenu naziona kuhusu album. Niwaambie tu, album itatoka mwezi 11 kwa sababu za kimsingi kabisa. Tumalizie some colabo na maandalizi ya album yenyewe. Tungependa kutoa burudani kipindi tulivu na rahisi kwetu. Thank you, tuendelee ku-enjoy muziki mzuri,” aliandika Nandy.

Ujumbe huo umeibua hisia mseto kutoka kwa mashabiki, baadhi wakionyesha hamu yao ya kusikia kazi mpya kutoka kwa msanii huyo ambaye kwa muda mrefu amekuwa mstari wa mbele katika kukuza muziki wa Tanzania kimataifa.

Hadi sasa, Nandy hajataja jina rasmi la albamu hiyo, lakini vyanzo vya karibu vinaeleza kuwa itakuwa miongoni mwa kazi zake kubwa zaidi, ikiwahusisha wasanii wa ndani na wa kimataifa.