
Timu ya taifa ya Nigeria, maarufu kama Super Eagles, imepata pigo kubwa wakati ikiendelea kujiandaa kwa mechi yao ya mwisho katika Kundi D ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), kufuatia taarifa kwamba beki wao tegemeo, Stephen Manyo, hatacheza kwenye mchuano huo dhidi ya Congo.
Manyo, ambaye ni mchezaji wa klabu ya Rivers United, aliumia bega katika mazoezi wiki iliyopita, na madaktari wamethibitisha kuwa hatakuwa fiti kwa ajili ya mechi hiyo inayotarajiwa kuchezwa usiku wa leo.
Hata hivyo, mechi hiyo haina uzito mkubwa kwa upande wa Nigeria, kwani tayari wametolewa kwenye michuano hiyo kufuatia matokeo mabaya katika mechi zao za awali. Kwa upande mwingine, Congo bado ina nafasi ya kufuzu hatua ya robo fainali, hivyo ushindi dhidi ya Nigeria ni wa muhimu sana kwao.
Katika mechi nyingine ya kundi hilo, Sudan itavaana na mabingwa watetezi Senegal kwenye Uwanja wa Amani, ulioko mjini Zanzibar. Sudan wanahitaji ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kuendelea katika hatua inayofuata ya michuano hiyo.