Msanii wa Uganda Nina Roz amepuzilia mbali kauli ya aliyekuwa mpenzi wake, Daddy Andre, aliyedai hatatoa msaada wowote katika kampeni zake za kisiasa iwapo hatalipwa.
Kwenye mahojiano ya hivi karibuni, Nina Roz amesema kuwa Andre hana mchango wowote katika safari yake ya kisiasa na kwamba hahitaji msaada wake kwa njia yoyote. Msanii huyo ameonyesha kutopendezwa na kauli hiyo na kueleza kuwa hana muda wa kujibizana na mtu ambaye hana nafasi katika mipango yake.
Ameongeza kuwa kuingia kwake katika siasa hakutamzuia kuendelea na kazi ya muziki, akibainisha kuwa ataendeleza vipaji vyake vyote viwili, kama alivyofanya Bobi Wine, ambaye pia alianza kama msanii kabla ya kuingia katika siasa.
Wikiendi iliyopita, Daddy Andre alieleza kuwa anaendesha muziki kama biashara na hatokuwa tayari kutumbuiza au kumpigia debe Nina Roz katika kampeni zake za Wilaya ya Sembabule bila malipo, akisisitiza kuwa anafanya kazi kwa misingi ya kibiashara.
Nina Roz, anayefahamika kwa wimbo wake maarufu “Billboard (Oliwa)”, aliteuliwa rasmi kuwa mgombea wa kiti cha Mbunge wa Wanawake wa Wilaya ya Sembabule katika uchaguzi mkuu ujao kupitia chama cha NUP chake Bobi Wine.