
Mwanamuziki kutoka Kenya, Nyashinski, ametangaza ujio wa album yake mpya ambayo kwa mujibu wake itakuwa na kiwango cha kimataifa.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Nyashinski amesema kuwa kwa muda mrefu amekuwa akiwaburudisha mashabiki wa Afrika Mashariki kupitia nyimbo zake, lakini sasa ameamua kupeleka muziki wake kwenye jukwaa la dunia.
Msanii huyo amefichua kuwa amekuwa akirekodi album hiyo kwa takribani miezi minane, na kwa sasa yupo kwenye hatua za mwisho kukamilisha video za nyimbo zitakazojumuishwa kwenye kazi hiyo.
Kwa mujibu wa tracklist iliyoichapishwa mtandaoni na Nyashinski, album hiyo inatarajiwa kuwa na jumla ya nyimbo 13, ikiwemo ngoma zinazojulikana kama Tai Chi na P.I.C. Amewataka mashabiki wake kujiandaa kwa safari ya kipekee ya muziki, akiwahimiza kuisikiliza album hiyo kuanzia wimbo wa kwanza hadi mwisho, akiahidi itakuwa tofauti na kazi zake za awali.
Hii inakuja wiki chache baada ya kujiunga na kampuni kubwa ya muziki, Sony Music, hatua inayotajwa kufungua milango ya kimataifa kwa safari yake ya kisanii.