
Mwanamuziki nguli wa Kenya, Nyashinski, amethibitisha kuwa albamu yake mpya itajulikana kwa jina “Yariasu” na itaingia sokoni tarehe 19 Septemba 2025.
Albamu hiyo inabeba jumla ya nyimbo 13, ambazo msanii huyo amezitaja kuwa za moto na zimeandaliwa kwa ubora wa kimataifa. Kupitia mitandao ya kijamii, Nyashinski amewataka mashabiki wake kufanya pre-order ya albamu hiyo mtandaoni ili kuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuisikiliza mara tu itakapotoka.
Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wake wameonekana kutaka zaidi, wakimhimiza kuachia albamu yote kwa pamoja badala ya kutoa ngoma moja moja. Licha ya maoni hayo, tayari Nyashinski ameachia nyimbo mbili kutoka kwenye albamu hiyo, ambazo ni “Tai Chi” na “P.i.c”, zilizopokelewa kwa shangwe na mashabiki wake.
Albamu ya “Yariasu” inatarajiwa kuwa miongoni mwa matoleo makubwa zaidi ya mwaka huu, ikidumisha nafasi ya Nyashinski kama mmoja wa wasanii wakubwa na wabunifu zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.