Msanii mkongwe wa Pwani, Nyota Ndogo, ameshindwa kuficha furaha yake baada ya kutimia kwa ombi lake la muda mrefu kufuatia kuachiwa kwa remix mpya ya wimbo wa Pawa ambayo Mbosso amemshirikisha rapa Khaligraph Jones.
Hii ni baada ya Mbosso kuzindua remix tatu tofauti za wimbo huo, akiwapa nafasi wasanii kutoka Tanzania, Rwanda na Kenya.
Kupitia Instagram, Nyota Ndogo ameeleza kuwa amefurahishwa sana na namna Khaligraph alivyoibeba kazi hiyo, akisisitiza kuwa hakumuangusha na kwamba remix hiyo imefikia matarajio aliyokuwa nayo. Lakini pia ameonekana kupuuza ukosoaji unaoweza kujitokeza, akisema kuwa kazi hiyo inastahili heshima kubwa.
Furaha yake imechochewa zaidi na ukweli kwamba miezi michache iliyopita aliwahi kutamka hadharani kuwa angependa kuona Mbosso akimshirikisha Papa Jones kwenye remix ya Pawa. Kauli hiyo ilimfanya Khaligraph kumtumia zawadi ya shilingi 100,000 za Kenya kama ishara ya kuthamini sapoti yake.