Rapa kutoka Kenya, Octopizzo, amezua mjadala mkubwa mitandaoni baada ya kutoa kauli tata kuhusu dini, hususan Ukristo.
Akizungumza kwa uwazi, Octopizzo amesema kuwa haamini katika dini ya Kikristo, akidai kuwa Ukristo kwa sasa umegeuzwa kuwa kitega uchumi na baadhi ya viongozi wa dini. Kwa mujibu wake, hali hiyo imemfanya kukosa imani na uhalisia wa dini hiyo.
Msanii huyo amesema imani yake imejikita zaidi katika ufahamu na utambuzi wa ndani, maarufu kama consciousness, akieleza kuwa mtu anaweza kuishi maisha yenye mwelekeo bila ulazima wa kufungamana na dini rasmi.
Aidha, Octopizzo amehoji kwa nini Ukristo una maelfu ya madhehebu ilhali waumini wote wanamwabudu Mungu mmoja. Ameeleza kushangazwa kwake na ukosefu wa umoja miongoni mwa Wakristo, akisema hali hiyo inaibua maswali kuhusu mshikamano na uhalisia wa imani hiyo.
Hakuishia hapo, rapa huyo pia amekosoa mwenendo wa kidini nchini Kenya, akidai kuwa Wakristo ndio kundi linalohukumu watu zaidi katika jamii, jambo analosema linakwenda kinyume na mafundisho ya upendo na uvumilivu.