Msanii wa muziki wa hip-hop kutoka Kenya, Octopizzo, ameikosoa vikali tabaka la wanasiasa nchini humo kwa kutoonyesha uwajibikaji katika matatizo yanayowakabili wananchi wa kawaida, hasa wafanyakazi wa sekta za umma.
Kupitia taarifa aliyoandika kwenye ukurasa wake wa X, Octopizzo amehoji kwa nini viongozi waliochaguliwa kama wabunge, maseneta na wawakilishi wadi hawajawahi kuandamana kudai mishahara yao inapochelewa, ilhali watumishi wengine wa umma mara kwa mara hulazimika kufanya hivyo.
Amebainisha kuwa kila mwaka, wataalamu muhimu kama madaktari, walimu na wahadhiri hulazimika kugoma au kuandamana kutokana na kucheleweshewa mishahara na mazingira duni ya kazi. Kwa mujibu wake, hawa ni watu wanaobeba mfumo wa afya na elimu wa taifa, na madai yao ni ya haki na muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Rapa huyo, amewataka viongozi kuchukua hatua za kweli kukabiliana na changamoto zinazowakabili wafanyakazi wa Kenya, badala ya kujikita katika maslahi binafsi ambayo hayaleti mabadiliko kwa wananchi wanaowawakilisha.
Octopizzo pia amewakumbusha viongozi wajibu wao wa kuhudumia umma, kulinda katiba na kuhakikisha huduma za serikali zinawanufaisha wananchi wote kwa usawa.