Others

Octopizzo Awataka Wakenya Wapunguze Hasira kwa George Ruto

Octopizzo Awataka Wakenya Wapunguze Hasira kwa George Ruto

Msanii maarufu wa muziki wa hip hop nchini Kenya, Octopizzo, amewataka Wakenya wapunguze hasira zao dhidi ya George Ruto, mwanawe Rais William Ruto, kufuatia uzinduzi wa matatu maarufu inayofahamika kama Nganya mwishoni mwa wiki hii.

Kupitia mitandao ya kijamii, Octopizzo amewakosoa Wakenya wanaomshambulia George kutokana na hali ya kiuchumi inayokumba taifa, akisisitiza kuwa “dhambi za mzee si za mtoi.” akimaanisha kuwa makosa au historia ya mzazi haifai kuhamishiwa kwa watoto wao.

“Dhambi za mzee si za mtoi,” aliandika msanii huyo, akisisitiza kuwa George ana haki ya kuishi maisha anayopenda bila kulaumiwa kwa sababu ya hadhi ya baba yake

Octopizzo pia ameelezea kuwa ni jambo la kawaida kwa mtoto wa bilionea kuishi maisha ya kifahari, akionekana kushangazwa na jinsi baadhi ya Wakenya wanavyomshinikiza George kutafuta kazi ilhali baba yake ana uwezo mkubwa wa kifedha.

 “Babake ni billionaire alafu mnataka George afanye kazi gani? Aanze kuuza mandazi?” aliandika kwa kejeli, akilenga kuonyesha kuwa ni kawaida kwa watoto wa viongozi matajiri kuwa na maisha ya kifahari.

Uzinduzi wa Nganya ya George Ruto ulifanyika kwa mbwembwe kubwa jijini Nairobi, huku baadhi ya Wakenya wakilalamikia matumizi ya kifahari wakati taifa linapitia changamoto za kiuchumi.